Na Thompson Mpanji
WATAALAMU wa
maji wamebainisha kuwa hadi kufikia mwaka 2022 wananchi wabonde la Ziwa Rukwa katika mikoa ya Mbeya na Rukwa watakuwa na upungufu mkubwa wa
mahitaji ya maji kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira hii si habari njema
hata kidogo kwa watanzania,wakati Serikali ya Tanzania inasema kufikia mwaka
2025 kila Mtanzania atakuwa na angalau unafuu wa maisha.
Kwa hivi sasa
imekadiriwa kuwa mtu mmoja wa bonde la Ziwa Rukwa anatumia
mita za ujazo 2250 kwa mwaka kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka
2002 ambapo idadi ya wakazi wa bonde hilo
walikadiriwa kufikia 2,168,240 ambapo inakadiriwa kuwepo na ongezeko
la wakazi mara mbili hadi kufikia wakazi 4,525,652.
Tafiti zinasema kuwa
kutokana na kuwepo kwa ongezeko kubwa la watumiaji wa maji mahitaji ya maji kwa
mtu mmoja kwa mwaka yatapungua hadi kufikia mita 1500 za ujazo kiwango
kinachodaiwa kuwa ni cha wastani kwa mujibu wa taarifa za kitaalamu za
kimataifa.
Hicho ni kiwango cha
wastani na kinadaiwa kuwa kikishuka chini ya hapo basi hali itakuwa mbaya sana
kwa binadamu,wanyama na viumbe vyote vilivyo hai kwa maana watu wanazidi
kuongezeka na hivyo mahitaji yanazidi kuongezeka lakini mazingira yanazidi
kuharibiwa na hivyo maji yanapunguwa na hatimaye kukauka kabisa.
Wataalamu wa maji
wanasema shughuli za binadamu kando kando ya mto zinatakiwa zianzie mita 250
kutoka ukingoni na Ziwa ni umbali ya
mita 500 lakini sheria za hamashauri na Serikali za mitaa zinasema umbali ni
mita kati ya 30 na 50 tu ebu angalia sheria hizo namna zinavyokinzana kwa hiyo
jamii imsikilize nani?.
Amini usiamini lakini
ndivyo ilivyo kuwa kina cha maji cha Ziwa hilo
kimepunguwa hadi kufikia mita mbili(mita 2)kwa mwaka 2006 na 2007 je kwa sasa
kitakuwa kimefikia wapi kwani ukiangalia kwa macho tu Ziwalinaonekana kuzidi kurudi ndani na kwamba hali hiyo inatokana
na Ziwahilo kujaa matope na taka nyingi,lakini pia maji yamepunguwa kwa
kiasi kikubwa kutoka usawa wa ardhi hadi kufikia mita zaidi ya 300 kuingia
ndani ya Ziwa kwa mwaka huo.
Kwa ujumla Ziwa Rukwa lina
umuhimu mkubwa kwa mahitaji ya binadamu na viumbe,mathalani ;Hifadhi za Taifa
zilizopakana na Ziwa hilo kama
Katavi,Rungwa,Rukwa na Lukwati
zinategemea sana kipindi cha kiangazi kuendeleza unyevu na matumizi ya
kurutubisha uoto wa asili.
Shughuli za usimamizi
wa rasilimali za maji katika mabonde zipo kwa mujibu kwa mujibu wa sheria namba
42 ya mwaka 1974 na sheria ya marekebisho namba 10 ya mwaka 1981,lakini je
zinasaidia vipi katika kutunza na kuhifadhi mazingira ya bonde la Ziwa Rukwa na kulinusuru na hatari ya kukauka
na kuleta madhara makubwa kwa binadamu na viumbe vilivyo hai
vinavyotegemea ikolojia ya Ziwa hilo?.
Wizara ya maji
kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wameamua kuketi kwa muda wa siku
mbili katika ukumbi wa mikutano wa Mkapa,uliopo Soweto,jijini Mbeya
wakishirikiana na watumiaji wa maji katika Mikoa mitano
inayopitiwa bonde la Ziwa Rukwa
ambayo Mbeya,Katavi,Rukwa,Tabora na Singida.
Ofisa wa maji bonde la Ziwa Rukwa,Florence Mahay amesema wameamua kukutana na wadau
mbalimbali waliopo ndani ya bonde hilo ili kupokea taarifa ya utafiti shirikishi wa matumizi
bora ya rasilimali maji na kuangalia njia mbadala ya kuhakikisha
wanafanya juhudi za kulinusuru bonde hilo ingawa kwa mujibu wa taarifa za watafiti kuwa
kwa sasa kuna kiasi kikubwa cha maji.
"Kwa ujumla kuna
uchafuzi mkubwa na uharibifu wa mazingira katika bonde la Ziwa Rukwa,watu wanalima kando ya Ziwa na mito,wafugaji wanachungia mifugo yao katika maeno
hayo,ukataji wa miti ovyo katika bonde,matumizi mabaya ya kemikali katika uchenjuaji wa madini na hasa
aina ya dhahabu na masuala shughuli nyingine za kibinadamu zinachangia
kuhatarisha ukosefu wa maji,"amesema.
Mwandishi wa makala hii amezungumza na Ofisa mipango
wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda Fosfan Nsuli ambapo ameelezea
hofu yake ya kutoweka kwa wanyamapori waliopo katika Bonde la Mto Katuma katika hifadhi ya
Katavi ambapo wanyama kama Viboko na mamba wakiwa na hali mbaya
kutokana na kujikuta wakiwa wamerundikana katika bwawa moja lenye matope
huku wakijisaidia haja kubwa na ndogo humo humo.
Hata hivyo Profesa
Japhet Kashaigile kutoka Chuo kikuu cha Sokoine amesema kuwa warsha
hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa jamii kujuwa umuhimu wa kutunza
rasilimali maji kwa ajili ya mazingira huku Prof Aris
Georgakakos kutoka Taasisi ya Gorgia institute of
Technology akitoa wito kwa jamii kuzingatia yale waliyowaeleza kwa
afya ya maisha yao.
"Ni vema wananchi
wakazingatia kile tulichowafundisha katika kuhakikisha wanatunza na
kuhifadhi mazingira,maji yatakuwa mengi,safi na salama na radha nzuri,na
huu ni utafiti wa awali tu lakini tunaendelea na utafiti ili tuweze
kubaini kiasi cha maji kilichopo ingawa kwa sasa maji ni mengi na ya
kutosha,"amesema Aris.
Profesa huyo amesema
kuwa utafiti wanaoendelea nao utabaini mahitaji ya maji kwa
wananchi wanaoishi katika mikoa mitano na watakuja kukaa tena na
kuzungumza tena na watumiaji na wadau ikiwa ni njia ya ushirikishwaji jamii
kuhusu matumizi bora ya rasilimali maji.
Mwisho.